Taasisi ya K finance imeanzisha mkopo wa ada za shule kwa wanafunzi ili kupunguza makali ya upatikanaji wa fedha baada ya kuisha mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona.
Akizungumza na MTANZANIA leo Jumatano Julai 8 katika viwanja vya sabasaba, Mkurugenzi Mtendaji wa K-finance, Judith Minzi amesema lengo ni kuwasaidia wazazi na walezi kupata ada.
Amesema katika kipindi cha mlipuko wa corona shughuli nyingi za uzalishaji zilisimama hivyo kuleta changamoto ya upatikanaji wa fedha za ada.
“Katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya corona biashara nyingi zilisimama na vipato vilipungua hivyo tumekuja na suluhisho la kuwasaidia,” amesema Judith.
Amesema mkopo huo utaanzia Sh. 500,000 hadi Sh. milioni tano na utalipwa moja kwa moja shuleni.
“Atakachokifanya mzazi au mlezi akikidhi vigezo ni kutuletea akaunti ya shule na jina la mtoto nasi tutalipa ada ya mwaka mzima,” amesema Judith.
Judith amesema kutokana na kuwapo kwa ugonjwa wa corona wameweka mfumo wa mwombaji kuomba kupitia tuvoti ya taasisi hiyo.
“Mwombaji anaingia katika tovuti yetu ya Www.kfinance.co.tz popote alipo na kuingiza taarifa zake na zikashughulikiwa ndani ya saa 48,” amesema Judith.